Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Hujjat al-Islam Sayyid Ahmad Iqbal Rizvi, Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Waislamu wa Pakistan, katika kujibu kufunguliwa kwa kesi zisizo na msingi dhidi ya waombolezaji wa Muharram, amesisitiza kuwa hatua hizo zifutwe mara moja.
Amesema kuwa: Kuomboleza kwa ajili ya Sayyid al-Shuhadā (as) ni ibada yetu, na hatukubali aina yoyote ya zuio au shinikizo katika jambo hili, kwa masikitiko, katika baadhi ya mikoa ya Punjab na Sindh, majlisi na maandamano ya maombolezo yamekuwa shabaha ya vitendo vya dhulma, na kesi za uongo na zisizo na misingi zimefunguliwa dhidi ya waombolezaji.
Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Waislamu Pakistan, akitaja nafasi ya makundi ya kitakfiri katika kuchochea hatua hizo, amesema kwamba: Kesi hizi zimefunguliwa kwa uchochezi wa makundi yenye misimamo mikali kupitia kwa polisi, ilhali waombolezaji hawakuwa na hatia na walikuwa tu wakitekeleza ibada yao ya kidini.
Amesisitiza kuwa: Vitendo hivi si tu kwamba havikubaliki, bali pia vinakiuka uhuru wa kidini na haki halali za kisheria za wananchi. Maombolezo ni haki yetu ya kisheria, na hakuna chombo chochote kilicho na haki ya kuzuia jambo hilo.
Hujjat al-Islam Sayyid Ahmad Iqbal Rizvi, akihitimisha, amewataka viongozi wa serikali kufuta mara moja kesi zilizofunguliwa dhidi ya waombolezaji, na kuchukua hatua madhubuti za kuzuia kurudiwa kwa vitendo vya namna hii vya dhulma.
Maoni yako